Tuesday, July 13, 2010

BABU AKUTWA AKIFANYA MAMBO YA UCHAWI

Wanafunzi wa Shule ya wasichana Tabora wameingiwa na hofu kubwa baada ya mzee mmoja aliyefahamika kwa jina la Shija Maganga kukutwa amekwama katika mfereji wa bomba la maji ndani ya eneo la shule hiyo ulio karibu na mabweni yao, tukio ambalo lilizua kelele nyingi shuleni hapo na wasomi hao walilihusisha na mambo ya kishirikina.Wanafunzi hao walipozungumza na mwandishi wetu kwenye eneo la tukio wiki iliyopita, walidai kuwa kwa siku kadhaa wamekuwa wakihofia wachawi kutokana na kusikia kelele usiku na wamejawa na hofu kwa kuwa katika shule yao kuna walemavu wa ngozi (Albino) na wamekuwa wakiiomba serikali kuwawekea uzio lakini ombi lao linapuuzwa.Mzee Maganga anayekadiriwa kuwa na miaka 80 aligunduliwa saa za asubuhi wakati afisa mmoja kutoka shirika linaloshughulikia masuala ya wakimbizi duniani la UNHCR anayesimamia ujenzi wa miundombinu ya majengo na maji, miradi inayofadhiliwa na shirika hilo, alipokuwa akiangalia ujenzi unavyoendelea pembezoni mwa mabweni shuleni hapo.Katika hali ambayo ni vigumu kuamini haraka, mzee huyo ambaye alishuhudiwa na umati wa watu wakiwemo wanafunzi wa shule hiyo, alionekana akiwa kwenye mfereji huo wenye upana wa kati ya sentimeta 25 na 27 (kama mwanandani wa kaburi) huku nyasi zikiwa zimezagaa juu ya mwili wake na alionekana akiwa mithili ya maiti, kitendo kilichomtia hofu afisa wa UNHCR.Kuonekana kwa mzee huyo kulizusha hofu miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo ambao baadhi yao walikuwa wakipiga kelele za ‘mchawi, mchawi’ huku wakibubujikwa na machozi.Baadhi ya wanafunzi walisikika wakidai kuwa wamemuona mwanga na huku tukio hilo likiendelea kuhusishwa zaidi na imani za kishirikina, hali iliyotokana na kuwepo kwa matukio mengine yanayofanana na hilo ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara katika shule hiyo ambayo ipo jirani na maeneo ya makazi ya watu.Aidha, baadhi ya wanafunzi walioshuhudia tukio hilo walisema walijisikia vibaya baada ya kumuona mzee huyo akiwa katika eneo lao kwa sababu hakuwa na maelezo ya kwanini alikutwa hapo na sababu zilizomfanya ajifiche kwenye majani.Wameendelea kuilalamikia serikali juu ya kuweka uzio katika shule yao jambo ambalo limekuwa ni kilio cha muda mrefu kisichosikilizwa na mamlaka husika.``Jamani kwa kweli serikali ingeliangalia tatizo hili la uzio ambalo ni la muda mrefu kwani tumekuwa tukiishi kwa mashaka makubwa, huyu mzee hatujui alikuja kwa nia gani au kama ni mwanga na alikuwa na nia ya kuturoga, ukweli hatuujui maana anasema alikuwa katika shughuli zake, tunajiuliza kwenye shughuli akiwa tumbo wazi tena usiku?” Alihoji mwanafunzi mmoja aliyeomba jina lake kutoandikwa gazetini.Mwanafunzi mwingine alisema wanatishika sana inapotokea mambo kama hayo kwani wana walemavu wa ngozi shuleni hapo, “Tunao wenzetu hapa shuleni ambao ni walemavu wa ngozi, albino, kuonekana watu kama hawa kunatutia wasi wasi sana na ndiyo maana tunadai kuwa tunawindwa na wanga.” Hata hivyo, gazeti hili lilipata fursa ya kuzungumza na mzee huyo kabla ya askari wa pikipiki wa jeshi la polisi maarufu PT kuwasili ambapo alitoa maelezo ya kutatanisha.Alipoulizwa na mwandishi wetu kama anajihusisha na kuwanga kama wanavyodai wanafunzi wa shule hiyo alikwepa swali hilo na badala yake alisema kuwa alikuwa ametokea nyumbani kwake eneo la Kata ya Tambuka Reli saa 10 usiku na alikuwa anaelekea Tabora Kitete kufanya shughuli zake lakini akajikuta yupo kwenye mfereji huo pasipo kujua.Alipoulizwa shughuli zipi ambazo anazifanya saa 10 alfajiri, hakujibu kitu ingawa mzee Maganga akithibitisha kuwa alikuwa amemaliza muda wa siku nzima akiwa ndani ya mfereji huo pasipo mtu yeyote kujua.Hata hivyo, hali halisi ya ngozi ya mwili wake ilionekana kuwa huenda ikawa alikuwa amekaa kwa siku zaidi ya tatu katika mfereji huo na alikuwa akishindwa kujinasua kwani polisi walitumia nguvu kumchomoa.Mkuu wa shule hiyo hakupatikana kuzungumzia mkasa huo ulioshitua wanafunzi na watu wengi wa eneo hilo na polisi nao hawakusema chochote kuhusiana na mkasa huo

0 comments:

 
Design by Kwetu Bongo