Thursday, May 27, 2010

Uchawi Uchawi

Uchawi wa vitabu

Kwa wale wasomi wengi wa Lugha ya Kiarabu watakuwa tayari wameishajua nini ninataka kuongelea.Uchawi mwingi ambao upo hapa kwetu unaoitwa uchawi wa vitabu na hutumiwa sana na baadhi ya watu kuumiza wenzao na kuwagombanisha au kuwaachanisha kati ya mke na mume, kuwagombanisha ndugu, kuwatupia majini watu, kuwapa nuksi na mengine mfano wa hayo.
Kuna watu huwa Mungu kawajaalia kuwa na akili mashuleni ila inapofikia kipindi cha Mitihani hufeli vibaya sana na wanakuwa wanaishia mitaani, katika hawa huingia mambo ya madawa ya kulevya, uvutaji bangi , ujambazi na unyang’anyi na mengine mengi ya ajabu na aibu.Mengi katika haya hutokana na uchawi wa kijini na uchawi unaotumia vitabu au uchafu.
Suali letu , uchawi huu wa vitabu asili yake ni wapi?
Ukitizama sana vitabu hivi vingi vimeandikwa kwa Lugha ya Kiarabu, na hivyo kimakosa wengi wanaweza kufikiri ni Kuruani.La hasha, vingi katika vitabu hivi si Kuruani ila maandiko ya makuhani wa Kigiriki(wayunani), makuhani wa Kiyahudi , makuhani wa Kihindi(Kihindu) na pia Makuhani wa Kisuriyani waliowahi kuishi miji ya Nineve na Babiloni(miji hii imetajwa katika Kura’ani na bibilia )
Swali letu la msingi bado linaendelea, mbona basi vipo katika Kiarabu?
Kwanza ieleweke , Kiarabu kinahusishwa sana na Uisilamu, hivyo wengi wameingia makosani kusema kuwa uchawi huu ni uchawi wa Kuruani au uchawi wa Kiarabu.Kamwe huu si uchawi wa Kuruwani, kwani Kuruani inakataza matendo ya Kishirikina ikiwemo kumshirikisha Mungu na kiumbe chochote na mfano utaona Kuruani inaongelea suala la majini walivyoanza kufundisha uchawi katika miji ya Babiloni na Mungu akawapa watu wa Babiloni watu wenye sifa za Kimalaika walioitwa Haruti na Marut ili kuwafundisha hao watu hiyo elimu ila wakawaonya watu kuwa tunakufundisheni elimu hii lakini sisi hatujamuasi Mungu.Kwa nini hawa malaika walianza kufundisha watu uchawi ikiwa basi Kuruani inakataza uchawi?Walifanya hivyo ili kuwaweka watu sawa kuwa majini si Miungu wala hawana nguvu za Kimungu au muujiza na hizo nguvu hazikuwa nguvu za Kimungu au muujiza ila nguvu za Giza au mauzauza na hivyo kila mtu anaweza kufanya huo uchawi na hivyo kuwapa tahadhari wanadamu kuwacha kuwaabudu Mashetani kwa kuwaonyesha mazingaombwe yao ili wapate ukubwa wa Ki-Mungu.
Baada ya matukio haya ya Babiloni, watu wakaanza kuandika uchawi katika vitabu na kufundishana.Lugha kubwa iliyokuwa ikitumika kuandika vitabu hivi ni Ki-Suriani ambayo hivi sasa ni lugha ambayo imetoweka ila bado wapo watu hususan wenye kufuata mafundisho ya Kikiristo huko maeneo ya Mashariki ya kati huitumia lugha hii kwa ibada zao. http://www.syriac.talktalk.net/syriac_history.html
Baada ya ujio wa Mitume wengine wa Mungu katika taifa la Israel lugha hii iliendelea kuwa Lugha ya mawasiliano na Lugha ya Kimaombi na elimu ya vitabu vya uchawi na uganga viliandikwa katika lugha hii.
Baadae watu wa Israeli nao wakaanza kuandika elimu hii na wakaishjihisha kuwa ni moja katika elimu za dini ya Kiyahudi na wakaiita Kaballah au Qaballah.Wakachanganya elimu za Mungu na elimu za Makuhani wakuu toka Iqipti(Egypt) mara baada ya kukombolewa na Nabii Musa toka Misr.
Maingiliano ya Warumi ,Wa-Iqipt, watu wa Babiloni, Nineve, Wayahudi, Wa-ajemi(Persian) ukazaa mabadilishano ya elimu hizi za uchawi , maarifa ya kimaisha na ujuzi , mila na ustaarabu,, elimu za kitabibu na elimu nyingine nyingi ambazo hapa si mahala pake pa kujadili.
Warumi walikuwa wameathirika sana na Wagiriki ambao walibobea katika elimu za Nyota, elimu za tiba, elimu za majini(mizimu), elimu za Falsafa na kadhalika
http://www.iep.utm.edu/greekphi/

Dunia ikawa imezama katika giza la upotofu na ukweli, elimu za Ki-Mungu zikachanganyika na elimu za kishetani.Ikumbukwe kuwa elimu hizi ziliendelea kuandika kwenye vitabu na watu waliendelea kufundishana elimu hizi kwa simulizi na kujifunza maneno ambayo yalikuwa yanaminika yana nguvu kuita majini au viumbe vingine visivyoonekana.Bado elimu hizi ziliendelea kuandikwa katika lugha za Kisuriani , Kiyunani, Kiyahudi , Ki-Ajemi, kwa herufi za Ki-iqipt(Hieroglyph) na hata kwa lugha za Kihindi , Nabatean, Aramaik na maandishi mengi zaidi yalikuwa ya Kigiriki.
http://www.sacred-texts.com/jud/jms/jms19.htm

Mbona elimu hii ya uchawi iko katika maandishi ya Kiarabu?
Ni kweli tunaona hivi hii leo maandishi mengi ya elimu za uchawi na Matalasimu yako katika lugha za Kiarabu, kwa nini na tunaambiwa uchawi ni haramu katika Kuraani?
Baada ya kufa Mtume Muhammad (s.a.w) kulikuwa kuna tawala nyingi za ki-Khalifa na elimu hii ilikuwa haramu mtu kuwa nayo.Na watu wengi walikuwa wakiuwawa(ndio Hukm ya Kiisilamu juu ya mchawi) mpaka ilipofikia U-Khalifa wa Abbasia(Abbasid Khalifate) katika mwaka 832 AD, Khalifa Harun Rashid aliona kuna haja ya kuanzisha idara ya kutafsiri elimu toka katika lugha kuu zingine zilizokuwa zikitumika ktika elimu za Kitiba na maarifa mengine , ni wakati huu ndipo ilipoanzishwa Bayt al Hikma huko Baghdad na walikusanywa wataalamu wa elimu hizi na elimu nyingine wakiwemo kinaThabit Ibn Quraa ambaye hakuwa Musuilamu
bali mfuasi wa dini ya Sabian na maandishi yao yalikuwa katika lugha ya Kigiriki.Hawa wanaitikadi kuwa wanamfuata Nabii Idris(Enoch).Huyu Thabit ndio muandishi na mtunzi wa kitabu cha kiganga kinaitwa Ghayat al Hakim ambacho kilitafsiriwa na kasisi wa kikatoliki Marsilio Ficino na kukiita De Imaginibus na kitabu hiki kilikuwa kikipatikana sana nchi za ulaya na kujulikana kwa jina jingine kama Picatrix
http://www.renaissanceastrology.com/picatrix.html
http://www.renaissanceastrology.com/thabit.html
Ukuwaji wa Baitu al Hikma ilisaidiwa sana baada ya china kugundua na kuanza kutengeneza karatasi na kusambaza Baghdad na Andalusia(Spain, kusini mwa Italy/Sicily, Ureno na baadhi ya maeneo ya Ufaransa mpaka Al-Hambra.

Elimu hii ikaanza kuingizwa kwenye lugha ya Kiarabu na vitabu vingi vikawa vinachapwa kwa lugha ya Kiarabu ila matamshi yaliwachwa vilevile mfano Adonai Asw-bahut al Ushudaya(ambacho ni Kiyahudi) na matamshi kama Ashmakhin Namushalakhin Aqshamshqin ambayo ni lugha ya Kisirianiyah.
Pia kuna maombi mengi toka lugha hizi ambayo yapo kwenye vitabu hivi ambayo si maombi ya Kiarabu wala mafundisho ya Kiisilamu mfano kuna maombi yanaitwa Barhatiyah ambayo yasemwa ni Lugha ya Kisuriani na lugha hii kwa mujibu wa vitabu inasemwa ilitumika wakati wa Nabii Adam.Vilevile kuna maombi yanaitwa Lahutiyah na Mahutiyah , haya pia si maombi kwa lugha ya Kiarabu ila herufi zake zimewekwa katika lugha ya Kiarabu na matamshi haya yako kwenye lugha ya Kisuriani na Kiyahudi na mafundisho mengine ya Kipagani.
Katika vitabu hivi maneno ya kigeni, yaani maneno ambayo siyo ya Kiarabu hufanyiwa tarjumani au tafsiri kwa lugha ya Kiarabu ili msomaji awe anaelewa nini anasoma.Mfano ni majina haya ya Kiyahudi na haya ya Kisuriani
Mfano neon Ahujin hutafsiriwa sawa na Al-Ahad yaani Mungu ni mmoja
Katika majina haya inaandikwa kuwa yana nguvu za kufanya jambo lolote zuri au baya ikiwa utafuatiliza masharti yake ipasavyo, mfano kufuata mwendo wa saa kwa kutmia , matumizi ya mafusho sahihi na kufuatiliza mwendo wa mwezi.
Katika vitabu hivi, ulifikia wakati wa dola za Kiisilamu kuvichoma moto na kuwauwa wale waliokuwa wakivitumia au kuviandika na kuvisambaza.mpaka pale lilipotokea kundi la watu ambao leo hii wanafanana na Free Mason(Masunia) likijulikana kama Ikhwan al Safwaa ambao walikuwa wakifuata Uisilamu wa Kishia mrengo wa Ismailia. Wao ndio walianza kuvihifadhi vitabu hivi na walikuwa na fikra ya kusema kuwa Mungu anayeombwa ni mmoja awe anatajwa kwa Lugha ya Kiyahudi au Kihebrania ,Kigiriki, Kisuriani au lugha yoyote maadam ni Mungu huyohuyo Mmoja wa Kweli na Haki basi na afuatwe.Ndio maana katika vitabu hivyo utakuta maneno kama Iluuhim(Elohim) Aswbahuwt(Asvaht) Ahya sharahiya na mengine mfano huo kutoka katika dini ya Kiyahudi.Hawa Ismailia walikuwa wanaitikadi ya Perenialism(walichanganya dini zote za kimila na dini za kimapokeo kuwa sawa)
Hawa Ismailia walipata nguvu baada ya kushika mamlaka na kuanzisha ukhalifa wao wa Fatimia na wakawa makao makuu yao nchini Misr.
Unaweza kusoma zaidi kuhusu Ikhwan al Safa hapa http://www.iep.utm.edu/ikhwan-al-safa/
Elimu hii ya vitabu kama inavyofahamika imekuwepo kwa karne nyingi hata kabla ya kuja kwa Mtume Muhammad SA.W kama tulivyoona katika makala yetu imeingizwa katika lugha ya Kiarabu na wengi wenye kujua kusoma Kiarabu vitabu hivi kwao inakuwa rahisi kuvipata na kuvielewa ila ni vyema watu wakajifunza zaidi elimu za Kiroho(Tazkiyah na Tasawuf) na kutegemea maandishi ya kiroho zaidi kuliko kuingia katika elimu hizi kwani zina mashaka mazito na mitihani mikubwa mno. Mungu akitujaalia tutaendelea kukuleteeni makala majini ni viumbe wa namna gani?Uchawi ni kitu gani?jinsi ya kujikinga na majini na uchawi , kwa nini watu wanajihusisha na uchawi?Masuunia ni nani na wanafanya nini?
Hakkam Mzee

7 comments:

Anonymous said...

Nimeipennda sana makala hii,tunaomba utuletee zaidi

Anonymous said...

nimependa sana nawaomba tuleteeni sasa naanza kuelewa

Anonymous said...

should any one tell me if this is true

Anonymous said...

Upuuzi mtupu, huyo dogo anatesa tu hao wanyama bila sababu yoyote ya msingi. Anatakiwa ashitakiwe kwa kukiuka haki za wanyama.

Tumaini Kayange said...
This comment has been removed by the author.
Anonymous said...

Naomba email address yako Dr. Na namba ya simu

don_ innocent1 said...

Nimeipenda sana tupe mwendelezo tafadhali

 
Design by Kwetu Bongo