Saturday, June 12, 2010

DR.MANYAUNYAU,MAKALA

TIBA za jadi ni tiba zilizokuwa zikitumiwa tangu enzi za mababu zetu. Lakini tiba hizo kwa sasa zinatumiwa tofauti, kwani baadhi wameifanya kama biashara na kupoteza thamani ya aina ya tiba na hivyo wengi hukimbilia hospitalini.
Hivi karibuni nilifanikiwa kukutana na mganga wa jadi, Jongo Salum, maarufu kama Dk. Manyanyau ili niweze kujua sababu za mganga huyo kutumia paka wakati wa kutibu.
Dk. Manyaunyau alizaliwa Kigamboni, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, miaka 28 iliyopita, na kupata elimu yake ya msingi katika Shule ya Kigamboni na kuishia Darasa la Nne.
Sababu za kuingia kwenye uganga
Dk. Manyaunyau anasema katika familia yao asili ya bibi na babu zake wako katika fani ya uganga. Na katika makuzi yake alikuwa karibu na na babu yake mzaa baba, mzee Abdallah Nyambo.
“Kilichomvutia babu yangu kuwa karibu nami ni utundu niliokuwa nao na pia katika ndoto nilizokuwa nikioteshwa usiku. Zilikuwa zikitokea ukweli, kitendo kilichompa babu yangu moyo kwamba ndiye ninayefaa kurithi mikoba yake, kwani kuna wakati kulikuwa kukitokea msiba karibu na mtaani kwetu, nilikuwa naweza kutabiri kwamba ni nani kafariki na nikienda unakuta ni kweli.
“Kutokana na hali hiyo, babu alianza kunitumia nimsaidie kufunga dawa za wagonjwa waliofika nyumbani kwake kwa ajili ya matibabu. Hata hivyo, kazi hii binafsi nilikuwa siipendi na hata nilipofikia hatua ya kumtamkia babu kwamba siipendi, aliendelea kunipa wasia na kuniambia mambo haya yapo katika jamii tunayoishi, hivyo nisiogope,” anasilimua Manyaunyau.
Anasema tangu babu yake amwambie maneno hayo, hakuwa anajisikia vizuri mara kwa mara, kwani kuna kipindi alipokuwa na homa, babu yake alimwingiza kwenye ofisi yake ya utabibu na kumwekea tunguli kichwani na kupona. Kitendo hicho cha kupona kila alipowekewa tunguli kilimzidishia babu yake faraja na kumwambia kuwa mizimu inamuhitaji.
Na kumwambia kuwa katika maisha ili afanikiwe anahitajika kuingia katika mambo ya uganga na kama hatokubali anaweza kuwa chanzo cha kutokea kwa vifo katika kizazi chao.
Dk. Manyaunyau anasema siku moja akiwa kijijini kwa babu yake huko Chole Samvula, alipelekwa na babu yake kwenye matambiko na aliporudi nyumbani kwa mama yake Kigamboni alimweleza mambo ayoambiwa na babu yake ayafanye. Hata hivyo, anasema umri wake ulivyofikia wa kuandikishwa shule, mama yake alienda kumwandikisha lakini hakusoma kwa raha.
Kuna kipindi wanafunzi wenzake walimtenga na kumuogopa kwa madai kwamba alikuwa akitoa macho wakati yeye alijiona kawaida.
Dk. Manyaunyau anasema ilifika wakati watoto hao wakaenda kumsemea kwa walimu na wazazi, jambo lililokuwa sababu ya yeye kuamua kukatiza masomo yake akiwa Darasa la Nne. Baada ya kuacha shule Dk. Manyaunyau alikwenda kufanya kazi ya kupaa samaki eneo la Feri. Baadaye alifanya kazi ya ubebaji takataka katika masoko ya Buguruni Kwa Mnyamani, wilayani Ilala.
Baadaye alijidumbukiza katika kazi ya upigaji debe ambako pia hakukaa sana katika kazi hiyo. Aliamua kwenda kujiunga na kikundi cha sanaa cha Kaole ambako alikuwa akiigiza kama teja.
Dk. Manyaunyau anasema pamoja na kupenda fani ya uigizaji, lakini hakuwa na raha nayo kutokana na vitu vilivyokuwa vikimwandama katika mwili wake kumsumbua kwani ilifika wakati hadi akashindwa kuigiza vipande alivyopangiwa.
“Siku moja nikiwa katika kazi hiyo ya uigizaji, nilishikwa na homa kali halafu kukawa na vivuli vikinitokea na kunikumbusha maagizo niliyopewa na babu. Vilinisisitiza kuwa hakuna riziki yoyote ya kifedha nitakayoingiza kama sitokubali kazi ya uganga,” anasema.
Anasema ndipo alipoamua kurudi tena kwa babu yake kijijini Chole na kurithishwa mikoba hiyo ya uganga.
Jinsi alivyorithishwa mikoba
Siku hiyo babu yake alimpeleka porini na kumchimbia shimo refu, akamtumbukiza na kumfikia kisha kumwacha sehemu ya kichwa tu.
Baada ya hapo alimzungushia nyoka mkubwa aliyezunguka shingoni na alitakiwa akae sehemu hiyo na nyoka huyo kwa siku saba na kuletewa dawa kila usiku na alipokunywa alijihisi kushiba.
Dk. Manyaunyau anasema babu yake alikuwa akizungumza na nyoka yule kila alipofika eneo hilo, na baada ya siku saba kuisha alichanjwa chale miguuni na mikononi ikiashiria kwamba ndio kinga yake.
Kama vile haitoshi baada ya kuchanjwa, aliletewa paka watatu ambapo babu alimchinja mmoja kati yao na kunywa damu. Na yeye akapewa anywe kwa maelezo kwamba ndiyo nguvu yake itakayokuwa inamuongoza.
Baada ya kumaliza zoezi hilo, anasema alitokwa na jasho jingi na kutetemeka takriban dakika tano, mwili ulipokuwa baridi, babu yake alimtaka kula na maini ya paka.
Dk. Manyaunyau anasema baada ya kumaliza kula maini yale, akaanza kuona ulimwengu mwingine. Aliweza kuona watu wakiwa majumbani mwao wanafanya shughuli zao na babu yake kumwambia sasa ameshaiva kwa ajili ya shughuli ya uganga na kumkabidhi rasmi vifaa vya uganga.
Vifaa alivyopewa na babu aliambiwa kwamba vitampa uwezo wa kupambana na ndondocha, wachawi, misukule na kumtaka kuwasaidia watu watakaokuwa wamekumbwa na vitu hivyo.
Vilevile babu alimlisha kitu alichokiita azima kilichomfanya aanze kuona vitu vya ajabu kama vile wenye kucha ndefu, watoto wachanga wanalia, watu wengine wakiwa wamevalia vizuri ambapo aliambiwa kuwa hao ndio misukule na kanzia hapo ndio akawa mganga.
Kazi alizowahi kufanya
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam kazi ya kwanza anasema aliifanya maeneo ya Yombo Vituka ambapo alitoa wachawi. Anadai wakati huo bado watu walikuwa wagumu kumkubali na kumuona kama mwongo.
Kazi nyingine aliifanya Yombo Buza ambako baba mmoja alikuwa na mgonjwa aliyefunga kula kwa muda wa siku 25. Katika utabibu wake, Dk Manyaunyau aliwaambia kwamba mgonjwa wanayemuuguza siye na badala yake ndugu yao huyo yupo juu ya dari na miongoni mwa wanaomtesa ni baba yake mzazi.
Siku aliyotaka kumtibu mgonjwa huyo aliwataka watu wengi kujitokeza, ili washuhudie kile anachokifanya kuondoa dhana ya kutomuamini.
Siku ilipowadia alifika nyumbani kwa baba mwenye mgonjwa huyo na kuwakuta wametandika maturubai kuashiria msiba. Hata hivyo, anasema aliwaacha wakaenda kuzika na kuahidi kwenda kumtoa marehemu huko huko makaburini.
Alipofika kwenye kaburi lile alipiga ‘nyanga’ moja na kutoka mbwa aliyekuwa amening’inizwa. Mbwa huyo alikuwa akitoa harufu kali na baadaye kugeuka kuwa mtu, lakini kutokana na kuchukuliwa msukule kwa muda mrefu, hakuishi muda mrefu tangu afufuliwe na badala yake alifarikiUmaarufu mwingine anasema aliupata pale alipoenda kuagua katika Shule ya Sekondari Yombo Vituka ambako wanafunzi walikuwa wakianguka ovyo. Watu walianza kumuamini na kupata kazi sehemu mbalimbali. Moja ya kazi aliyopata Dk. Manyaunyau anasema aliitwa Mwananyamala kumtoa mtoto aliyepotea.
Baada ya kupatikana kwa mtoto huyo alipewa nyumba ya kuishi ili kuweza kutoa wachawi.
Magonjwa anayotibu
Mbali na kutoa mambo ya ajabu ajabu namna hiyo, lakini pia anatibu magonjwa mengine kama kisukari, pumu, ngiri, mgoro, kiarusi, malaria na magonjwa mengine
Anasemaje kuhusu mauaji ya albino
Dk. Manyaunyau anasema si kweli kwamba viungo vya albino vinatumika kazi katika kutibu. Amewaita watu wanaofanya hivyo kuwa ni majangili.
Anasema hakuna ukweli wowote kwamba utumiaji wa viungo vya binadamu ndiyo unaomfanya mtu apate mafanikio. Amewataka wanaoamini mambo hayo kuacha mara moja.
Akizungumzia kuhusu kufutiwa leseni waganga na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Dk. Manyaunyau anasema hiyo si njia pekee ya kupambana na vitendo hivyo. Badala yake serikali na waganga washirikiane katika kukomesha vitendo hivyo, kwani ukweli ni kwamba wao wenyewe wanajuana nani mganga wa kweli na nani si mganga.
Anasema kwa kusitisha huduma hizo za uganga kutakuwa ni mateso kwa watu ambao magonjwa yao yanatibiwa kwa dawa asilia.
Hata hivyo, anawataka watu wanaotumwa na waganga kupeleka viungo hiyo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, ili watuhumiwa waweze kukamatwa. Waganga wanaotumia viungo vya binadamu ndio wachawi

0 comments:

 
Design by Kwetu Bongo