Monday, June 14, 2010

DR.MANYAUNYAU MAZESE

Mganga maarufu jijini Dar es Salaam, Manyaunyau, akitafuta nyoka anayesadikika kuwa jini katika eneo la Manzese Midizini. Nyoka huyo wa 'ajabu' amesumbua wakazi wa Kata hiyo kwa kipindui cha zaidi ya wiki mbili na kugonga watu kimazingara. (Picha na Heri Shaaban)

HOFU imetanda miongoni mwa wakazi wa Manzese na vitongoji jirani baada ya kuibuka uvumi kuwa kuna nyoka anayewagonga watu kimaajabu katika njia inayopita kwenye makaburi yaliyopo Manzese Midizini.
Hali hiyo imewafanya wakazi wa maeneo hayo pamoja na wapita njia waliokuwa wakiitumia njia hiyo kulazimika kupitia njia nyingine, na pia wamelazimika kumuita mganga wa kienyeji, Jongo Seleman maarufu kama Dk. Manyaunyau, ili kuangalia kama atawasaidia wakazi hao kuondokana na hali hiyo ambayo wanahisi kuwa ni mambo ya mazingara.Baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameliambia gazeti hili kuwa tangu tatizo hilo lianze karibu wiki mbili zilizopita, wapitanjia saba katika eneo hilo wameshagongwa na nyoka huyo wa ajabu ambaye hubadilika rangi na umbo kila mara.Baadhi ya watu wanaodaiwa kugongwa na nyoka huyo ni Rose John wa Midizini, Manzese, ambaye ameliambia gazeti hili alivyogongwa na nyoka huyo wa ajabu. Ingawa hakuumia kiasi cha kulazwa hospitali, amesema amepatwa na mshtuko mkubwa.Mwingine anayedaiwa kugongwa na nyoka huyo ni Farida Hamza ambaye inadaiwa kuwa amelazwa katika Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu na Halima Hamisi wa Mazense Mzambarauni ambaye naye amegongwa.Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa wa Kata ya Mzambarauni, Ahmed Mteremko na Omari Pinde wa Kata ya Midizini, walipoulizwa kuhusu habari hizo, walisema hawajazithibitisha.Hata hivyo, Diwani wa kata hiyo, Kassim Lema, alishauri kuwa eneo lote hilo lisafishwe, jambo ambalo lilifanyika, lakini bado watu wanaendelea kugongwa na nyoka huyo kiasi cha kuwafanya baadhi ya wananchi wa eneo hilo kumleta mganga wa kienyeji ingawa viongozi wa mtaa huo walikataa wakidai kuwa Serikali haiamini ushirikina.Wananchi waliohojiwa na gazeti hili jana na leo wamesema nyoka huyo amekuwa akijitokeza katika ukubwa mbalimbali huku akiwa katika rangi tofauti hali ambayo imekuwa ikiwafanya waamini kuwa nyoka huyo siyo wa kawaida."Kabla hajakugonga, kwanza kinakuja kitu kama mfuko laini wa nailoni unaopeperushwa na upepo, halafu unajiviringisha mguu ukija kutaamaki ni nyoka," amesema mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Asha Ramadhan.Amesema nyoka huyo akishamgonga mtu hutoweka tena katika mazingira hayo hayo ya kutatanisha na kwamba kutokana na hali hiyo, wakazi wa eneo hilo wamewazuia watoto wao kupita njia hiyo wakati wa kwenda na kutoka shule kwa hofu ya kugongwa na nyoka huyo.Naye Yusuf Ramadhan, mkazi wa Manzese, amesema hali hiyo imewafanya waishi kwa hofu kwa sababu hawajui kitakachotokea baadaye.Amesema tatizo hilo lilianza wiki mbili zilizopita na kadiri siku zinavyopita ndivyo hali ya wasiwasi imekuwa ikizidi kuongezeka."Kwa kweli hali ni ya kutisha na njia hii ndiyo ilikuwa rahisi kwenda maeneo mbalimbali kama Mabibo lakini inatubidi tusipite," amesema Ramadhan.Gazeti hili lilipofika eneo hilo jana walikuta umati mkubwa wa watu ukiwa umeandamana na Dk. Manyaunyau ambaye alikuwa akijaribu kutumia njia za asili ili kujaribu kumkamata nyoka huyo.Hata hivyo, mganga huyo alionekana kuelemewa baada ya kuwaeleza wakazi hao kuwa mambo aliyoyaona ni makubwa na hivyo inamlazimu akakusanye nguvu zaidi na kuwaahidi kurejea eneo hilo leo.Imani za kishirikina zimekuwa zikiibuka mara kadhaa jijini na kuwafanya watu kuishi kwa hofu.Miongoni mwa imani hizo ni pamoja na ile ya kuwepo mdudu anayeitwa ‘Popo Bawa’ ambaye anadaiwa kuwaingilia watu kimazingara

0 comments:

 
Design by Kwetu Bongo